Mwisho wa karne ya 17, Bwana Wetu
alimtokea Mtakatifu Margaretha Maria Alakoki (1647-1690) na kumwomba aeneze Ibada
kwa Moyo Wake Mtakatifu. Katika barua aliyomwandikia Mkuu wa Shirika lao mwezi
Mei 1688, Mtakatifu Margaretha Maria alimueleza kuhusu kile kinachoitwa “Ahadi
Kuu ya Bwana Wetu” kwa wale watakao fanya Ibada ya kulipia kila Ijumaa ya Kwanza ya mwezi kwa miezi tisa mfululizo
pia Bwana wetu alimwambia juu ya nini tunapaswa kufanya ili kuipata ahadi hiyo,
Bwana wetu alimwambia Mtakatifu Maria Alakoki:
“Kwa sababu ya huruma
kubwa mno ya Moyo wangu nakupa ahadi, ya kwamba mapendo yangu yenye enzi
yatawapa wote wenye kupokea komunio Takatifu Ijumaa ya kwanza ya mwezi kwa
miezi tisa mfululizo neema ya kutubu saa ya mwisho; hawatakufa katika hasira
yangu, wala bila sakramenti; Moyo wangu wa kimungu utakuwa kimbilio lao katika
kufa kwao.”
Sasa baada ya kusikia Habari ya ahadi
kubwa. Najua utakuwa unajiuliza: “Nifanye nini, ili nipate mazao ya ahadi hiyo
kubwa?”.
Kwanza kila mmoja, apendaye kushirikiana
katika mazao hayo ya ajabu hana budi kuipokea komunio ya kutuliza Ijumaa ya
kwanza ya mwezi kwa miezi tisa mfululizo.
Watu wengi wataona shida sana kushika
ijumaa tisa za kwanza. Lakini hilo litawezekana tu iwapo ukifanya juhudi kubwa.
Lakini bora ufanye juhudi kubwa, kwani hata katika hali ya kawaida unapotaka
kununua kitu cha thamani kubwa ni lazima ufanye kazi kwa bidii ili upate pesa
kwa ajili ya kununua kitu hicho. Basi ukitaka kupata ulinzi wa pekee wa Mungu
saa ya kufa na matumaini makubwa ya kuingia katika uzima wa milele, hutalegea
kufanya juhudi kubwa. Utakuwa tayari kuzishinda shida na kulipa kwa sadaka zako
. hutaogopa mvua, wala taabu yoyote, bali utafurahi kujitolea sadaka.
Utamkumbuka Yesu aliyekwenda njia ya msalaba siku ya ijumaa kuu, nawe utatamani
kumfuata kwa mapendo. Siku za kutimiza masharti ya kupata mazao ya ahadi kubwa
utajaa furaha na tulizo.
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni mwema mno. Nao
hufurahishwa pia na komunio ya kutuliza ipokewayo siku ya Dominika. Tena Yesu atawalipa wenye
kuipokea siku hiyo, kwa maana hisani yake haina mipaka. Lakini ukitaka kuyapata
mazao ya ahadi kubwa kwa hakika, huna budi kupokea komunio Takatifu ijumaa ya
Moyo Mtakatifu wa Yesu, yaani siku iliyowekwa na Bwana Yesu mwenyewe.
Hata kama mtu ameanza kuzishika Ijumaa
tisa za kwanza na amekosa nafasi ya kupokea Komunio Takatifu Ijumaa moja ya
katikati, hana budi kuanza upya tena.
Ila watu wasiopata nafasi yoyote
kuzishika Ijumaa, waipokee Komunio ya Kutuliza Dominika badala yake. Nao
waitumaini hisani ya Bwana Yesu atakayewagawia katika wingi wake.
Pili, wenye kushika Ijumaa tisa za Moyo
Mtakatifu wa Yesu hawana budi kupokea Komunio Takatifu katika hali nzuri tena
kwa kusudi lililotajwa na Yesu, yaani kufurahisha Moyo wake Mtakatifu, na
kuulipa makosa ya watu. Basi ukitaka kuyapata mazao ya ahadi kubwa, usisahau kufanya maungamo kwa padre na kuweka kusudi
hilo kabla ya kupokea komunio ya kutuliza.
Pia unaweza kusali sala ifuatayo baada ya
kupokea komunio ya kutuliza:
Ee Yesu, wewe u rafiki yangu na mkombozi
wangu. Lakini ole wangu, nilifanya nini? Nilikudharau Mara nyingi. Nilikuwa
kama kibarua anayengoja amri tu bila bidii yake mwenyewe. Hata amri zako nilizishika nusu tu. Nawe umeningojea kwa uvumilivu. Leo unaniita tena nikupende vile rafiki anavyompenda rafiki.
Toka leo nitaitikia mapendo yako kwa
mapendo. Kwa hiari yangu nitshika ijumaa ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Nitapokea
komunio takatifu siku hiyo, ili niufurahishe Moyo wako na kulipa makosa
unayokosewa na watu.
Kabla ya kupokea komunio ya kutuliza
nitaweka kusudi hili:
“Bwana wangu, sasa nataka kupokea Komunio
Takatifu, ili nikurudishie mapendo na kukufariji kwa ajili ya ubaridi wote na
dhambi zote ulizokosewa na watu katika sakramenti ya mapendo.”
Ee Yesu nakuomba, unipe nguvu nishike
kusudi hilo. Nami najua ya kuwa wewe utashika maneno yako uliyomwambia
Mtakatifu Margareta Maria, ndiyo: “ Nitakuwa kimbilio lako katika Maisha na
hasa saa ya kufa”.
Moyo wa Yesu, matumaini yao wanaokufa
katika neema yako, utuhurumie.
Moyo wa Yesu, malipo kwa dhambi zetu,
utuhurumie.
0 Comments