Nuru ya Maria · Tafakari
Mtikisiko Katika Kanisa: Maaskofu, Amri ya Papa, na Hatari ya Uasi
Kwa nini umoja na Kiti cha Petro ni muhimu kuliko mapokeo pekee.
Kama unavyojua, Kanisa Katoliki ni moja, takatifu, la kitume, na linaongozwa na kiongozi mmoja ambaye ni Khalifa wa Mtakatifu Petro — Baba Mtakatifu Papa. Sasa, kuna kitu kimetokea ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika Kanisa kwa karibu miaka 40 iliyopita.
Kikundi cha Kikatoliki cha Kijadi kijulikanacho kama SSPX (Society of St. Pius X) kule Uswisi, kimeamua kuweka wakfu maaskofu wanne wapya bila idhini ya Papa Leo XIV, kinyume kabisa na maonyo na ombi lake la kibinafsi.
Kisheria na kikanuni (Canon Law), kitendo hiki kinabeba adhabu ya moja kwa moja ya kutengwa na Kanisa (Automatic Excommunication). Vatican imekitaja kitendo hiki kama “Uasi” (Schismatic Act).
Moyo wangu unauma kwa sababu najua vijana wengi wanaopenda Misa za Kilatini, mapokeo ya kale, na unyofu wa kiimani wanajikuta njia panda. Hebu tushuke chini kidogo kuelewa kwa upendo na ukweli: nini kimetokea, kimetoka wapi, na sisi kama waamini wa kweli tusimame wapi?
Asili ya Jeraha: Askofu Mkuu Marcel Lefebvre
Ili kuelewa kwa nini SSPX wamefanya hivi, lazima umfahamu muasisi wao, Askofu Mkuu Marcel Lefebvre wa Ufaransa. Alikuwa mmisionari mkubwa sana Afrika (hasa Senegal). Alikuwa mtu aliyependa Kanisa kwa dhati, lakini alilelewa kwenye misingi ya kale kabisa ya kabla ya Mtaguso wa Pili wa Vatican (Vatican II).
Wakati Mtaguso wa Vatican II ulipomalizika mwaka 1965, mabadiliko yalikuwa makubwa: Misa zikaanza kusomwa kwa lugha zetu (kama Kiswahili), altare zikageuzwa kuwatazama waamini, na Kilatini kikapotea taratibu. Lefebvre aliona kama mabadiliko haya yanaharibu ukweli na uzuri wa Kanisa. Mwaka 1970 akaunda kikundi cha SSPX ili “kutunza mapokeo ya kale.”
Mvutano ulienda mbali hadi mwaka 1988, ambapo yeye (akiwa na umri wa miaka 82) aliamua kuweka wakfu maaskofu wanne bila ruhusa ya Papa Yohane Paulo II. Papa alimsihi asifanye hivyo, lakini alikaidi. Matokeo yake yakawa ni kutengwa (Excommunication), na akajenga ukuta mkubwa kati ya shirika lake na Vatican.
Kilele cha Leo: Kwa Nini Wamerudia Kosa Lile Lile?
Maaskofu waliobaki wa SSPX sasa hivi wameshazeeka (mmoja ana miaka 80 na mwingine 69). Bila maaskofu wapya, hawawezi kupata mapadri wapya, na kikundi chao kitakufa. Ndiyo maana wametumia hoja ya “Hali ya Dharura” kusimika maaskofu hawa wanne wapya.
Baba Mtakatifu Papa Leo XIV na Baraza la Vatican wamekuwa wavumilivu sana. Milango ilikuwa wazi kwa miezi kadhaa, mazungumzo yalifanyika, lakini SSPX walitoa barua ya wazi wakisema wanakataa mambo kadhaa ya Vatican II, na kwamba “wako tayari kufa kuliko kuacha misingi yao.” Na kweli, wakakaidi na kuweka wakfu hao maaskofu.
Watu wa SSPX Si Wabaya — Hapa Ndipo Palipo na Utata
Ndugu yangu, nataka niwe mkweli kwako. Watu wanaokwenda kusali kwenye makanisa ya SSPX siyo watu wabaya au wahalifu. Ni Wakatoliki wenzetu, wacha Mungu sana, wanaopenda utakatifu, wanapenda Rozari, wanalelewa kwenye mafundisho magumu kuhusu dhambi, motoni na utakatifu, na seminari zao zimejaa vijana. Wanatamani kuona Kanisa linalosimama imara bila kuyeyushwa na ulimwengu wa sasa.
Hamu hiyo ni halali kabisa — hata mimi na wewe tunaitamani! Lakini hapa ndipo shida inapoanza: umoja na Papa siyo chaguo la fasheni au staili. Siyo kitu unachoweza kukiweka pembeni eti kwa sababu tu hukubaliani na mwelekeo wa sasa wa Roma.
Habari Njema: Huna Haja ya Kuchagua Kati ya “Mapokeo” na “Papa”
Kama unapenda Misa ya Kilatini yenye heshima kubwa, ukimya mtakatifu, na uzuri wa kale — habari njema ni kwamba unaweza kuipata hiyo NDANI ya Kanisa Katoliki lililo chini ya Papa.
Baada ya uasi wa mwaka 1988, mapadri wengi walikataa kumfuata Askofu Lefebvre kwenye uasi. Walitoka na kuunda shirika linaloitwa FSSP (Priestly Fraternity of St. Peter).
FSSP wanasoma Misa ileile ya kale ya Kilatini, wanavaa mavaz ya kale katika misa zao, wana misingi ileile thabiti ya kiimani, lakini wapo katika umoja kamili (Full Communion) na Papa. Hawakuvunja sheria. Hakuna sababu ya kukimbilia makundi yasiyo na uhusiano rasmi wa kisheria na Vatican (irregular canonical status) wakati Kanisa mama linakupa nafasi ya kusali kwa unyofu na heshima ndani ya nyumba.
Wito Wangu Kwako Mwezi Huu
Kitendo kilichotokea kinaleta maumivu makubwa kwa kila anayelipenda Kanisa. Marcel Lefebvre hakuwa mtu mbaya; alikuwa mtu aliyependa Kanisa kiasi cha kuchagua kulilinda kwa njia yake mwenyewe badala ya utii. Lakini historia inatufundisha kuwa hakuna matunda mema yanayozaliwa nje ya utii kwa Kiti cha Petro.
Mwisho wa siku, usiku ule wa Alhamisi Kuu kabla ya kufa, Yesu hakusali tu kwamba tuwe wasafi au wa kimapokeo pekee; alisali:
“Wote wawe wamoja… kama sisi tulivyo wamoja.”
— Yohane 17:21Hebu mwezi huu tusali kwa ajili ya:
- Mapadri na waamini wa SSPX walioko kwenye mtikisiko huu sasa hivi.
- Baba Mtakatifu Papa Leo XIV, anayebeba msalaba huu mzito kwa unyenyekevu na upendo wa kichungaji.
- Umoja wa Kanisa letu, ili kusiwepo na mifarakano.
Je, una mtazamo gani kuhusu mtikisiko huu katika Kanisa letu leo? Tuandikie maoni yako hapa chini — na tusisahau kuombeana kama ndugu wa familia moja ya Kristo.
0 Comments