Sala · Ibada ya Maria
Rozari Takatifu
Mwongozo kamili: namna ya kusali, matendo, Litania, na sala ya Kumbuka.
Rozari Takatifu ni sala yenye nguvu na maarufu sana katika Kanisa Katoliki. Husaliwa na Wakristo kutafakari maisha ya Yesu na Maria — yaani Fumbo la Ukombozi — hasa kipindi cha mwezi Mei na Oktoba. Inahimizwa kuisali kama familia kila siku.
Tusali Rozari tupate amani, wakosefu waongoke, na wasiomjua Yesu Kristo wamjue na kuokoka.
Namna ya Kusali Rozari
Ishara ya Msalaba. Anza kwa kuibusu miguu ya Bwana Yesu katika picha yake Msalabani, kisha fanya Ishara ya Msalaba ukigusisha msalaba wa Rozari kwenye paji la uso, kifuani, bega la kushoto na la kulia, huku ukisema: “Kwa Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.”
Taja nia zako. Tangaza nia zako kwa ufupi. Kama mnasali wengi kwa pamoja, zitamke kwa sauti. Mfano: “Tusali kuombea amani katika nchi yetu na ulimwenguni kote”, au “Tutolee Rozari hii kuwaombea wagonjwa wetu.” Au unaweza kutoa nia kuendana na tendo la fungu husika la Rozari.
Kanuni ya Imani. Baada ya kutoa nia, sali sala ya Kanuni ya Imani:
Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi, mwumba mbingu na dunia. Na kwa Yesu Kristo, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu; aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu; siku ya tatu akafufuka katika wafu; akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi; toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa Takatifu Katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili, uzima wa milele. Amina.
Baba Yetu. Kwenye punje kubwa inayofuata, sali sala ya Baba Yetu:
Baba Yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe; ufalme wako ufike; utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku; utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.
Salamu Maria tatu. Katika punje tatu ndogo zinazofuata, tunamwomba Mungu (Utatu Mtakatifu) fadhila za Imani, Matumaini na Mapendo, kila ombi likiambatana na Salamu Maria:
• Mungu Baba, utuongezee Imani.
• Mungu Mwana, utuongezee Matumaini.
• Mungu Roho Mtakatifu, washa nyoyo zetu kwa mapendo yako.
Au: “Utuongezee Imani ee Bwana”, “Utuongezee Matumaini ee Bwana”, “Uwashe nyoyo zetu kwa mapendo yako ee Bwana.”
Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote. Na Yesu, Mzao wa tumbo lako, amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
Atukuzwe Baba. Katika punje kubwa inayofuata baada ya punje tatu ndogo, sali:
Atukuzwe Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina.
Tafakari fumbo la kwanza. Kila fungu la Rozari linahusishwa na fumbo la maisha ya Yesu au Bikira Maria. Anza na fumbo la kwanza, ulitafakari, kisha sali Baba Yetu kwenye punje kubwa.
Salamu Maria mara kumi. Ukiwa umeshika Rozari, sali Salamu Maria moja kwa kila punje ndogo, hadi kumi. Unaposali kila Salamu Maria, zingatia na utafakari fumbo ulilolitaja.
Atukuzwe Baba na sala ya Fatima. Kwenye punje kubwa inayofuata baada ya Salamu Maria kumi, sali Atukuzwe Baba, kisha sali:
Tuwasifu milele Yesu, Maria na Yosefu.
Ee Yesu wangu, utusamehe dhambi zetu, utukinge na moto wa milele, ongoza roho zote mbinguni, hasa za wale wanaohitaji zaidi huruma yako.
Taja fumbo la pili. Endelea na utaratibu uleule hadi fumbo lifuatalo, ukirudia hatua ya 7 hadi ya 9.
Endelea na mafumbo yaliyosalia. Rudia hatua ya 7 hadi 9 kwa mafumbo yote, ukitangaza kila moja kabla ya kusali Salamu Maria kumi.
Salamu Malkia. Baada ya kukamilisha miongo yote mitano, maliza kwa sala ya Salamu Malkia (Salve Regina):
Salamu Malkia, Mama mwenye huruma; uzima, tulizo, na matumaini yetu, Salamu! Tunakusihi ugenini hapa sisi wana wa Eva. Tunakulilia, tukilalamika na kuhuzunika bondeni huku kwenye machozi. Haya basi, Mwombezi wetu, utuangalie kwa macho yako yenye huruma; na mwisho wa ugeni huu, utuonyeshe Yesu, Mzao Mbarikiwa wa tumbo lako. Ee Mpole, ee Mwema, ee Mpendelevu, Bikira Maria.
Ishara ya Msalaba. Maliza Rozari kwa kufanya Ishara ya Msalaba: “Kwa Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.”
Matendo ya Rozari
Matendo ya Furaha
- Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie unyenyekevu.
- Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tumwombe Mungu atujalie mapendo ya jirani.
- Yesu anazaliwa Betlehemu. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara.
- Yesu anatolewa hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie usafi wa moyo.
- Maria anamkuta Yesu hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie kuwatii wakubwa wetu.
Matendo ya Uchungu
- Yesu anatoka jasho la damu kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie sikitiko la dhambi.
- Yesu anapigwa kwa mijeledi kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuacha dhambi za uchafu.
- Yesu anatiwa miiba kichwani kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kushinda kiburi.
- Yesu anachukua Msalaba kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuvumilia taabu.
- Yesu anakufa Msalabani. Tumwombe Mungu atujalie kuwapenda Yesu na Maria.
Matendo ya Utukufu
- Yesu anafufuka. Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.
- Yesu anapaa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kwenda mbinguni.
- Roho Mtakatifu anawashukia Mitume. Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.
- Bikira Maria anapalizwa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kufa vizuri.
- Bikira Maria anawekwa Malkia mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema.
Matendo ya Mwanga
- Yesu anabatizwa Mto Jordani. Tumwombe Mungu atujalie uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo.
- Yesu anageuza maji kuwa divai huko Kana. Tumwombe Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya Injili.
- Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie kupokea Ufalme wake kwa toba ya kweli.
- Yesu anageuza sura. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuung’arisha ulimwengu kwa uso wa Yesu.
- Yesu anaweka Sakramenti ya Ekaristi. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.
Litania ya Bikira Maria
— Utuhurumie —
— Utuombee —
— Mwanakondoo wa Mungu —
Ee Bwana Mungu, utujalie sisi watumishi wako afya ya roho na mwili siku zote; na kwa maombezi matukufu ya Maria Mtakatifu Bikira daima, tuopolewe na mashaka ya sasa, na tupate furaha za milele. Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Kumbuka
Kumbuka, ee Bikira Maria mpole sana, haijasikika kamwe kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, aliyeomba msaada na maombezi yako. Kwa matumaini hayo, nakukimbilia, ee Mama Mkuu wa Mabikira; naja kwako, nasimama mbele yako nikilalamika, mimi mkosefu. Ewe Mama wa Neno wa Mungu, naomba usikatae maneno yangu, bali uyasikilize. Amina.
0 Comments