Ulimwengu wetu una mambo mengi
yanayouma na kutatiza—chuki, vurugu, na kupotea kwa maadili. Wakati mwingine
tunaona hatuna nguvu ya kubadilisha chochote. Lakini Mungu ametupa silaha mbili
rahisi za kiroho: Moyo wa Yesu na Moyo wa Mama Maria.
Wengi wetu tunaijua ibada ya Ijumaa ya
Kwanza kwa ajili ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Lakini leo nataka nikupe siri ya
ibada pacha yake: Jumamosi Tano za Kwanza kwa ajili ya Mama Maria.
Shida ni Ipi?
Mwaka 1917, Mama Maria alitokea Fatima,
Ureno, kwa watoto watatu wachungaji. Alionya kuwa ulimwengu utapitia magumu
mengi kama wanadamu wasipokubali kutubu.
Mwaka 1930, Yesu alimweleza mmoja wa
wale watoto (Sista Lucia) kuwa Moyo wa Mama yake unajeruhiwa sana na aina tano
za makosa yanayofanywa na wanadamu:
- Watu
wanaokataa kwamba Maria alizaliwa bila dhambi ya asili.
- Watu
wanaokataa ubikira wake.
- Watu
wanaokataa kwamba yeye ni Mama wa Mungu na Mama yetu sote.
- Watu
wanaofundisha watoto wadogo kumdharau au kumchukia Mama Maria.
- Watu
wanaoharibu au kudhihaki sanamu na picha zake takatifu.
Kila mara watu wanapofanya mambo haya,
ni kama wanachoma miiba kwenye moyo wa Mama Maria. Ibada hii ipo ili kuiondoa
hiyo miiba na kumfariji mama yetu Bikira Maria.
Unatakiwa Kufanya
Nini? (Mambo 4 Tu)
Ili kufanya ibada hii, unachotakiwa
kufanya ni kutenga Jumamosi ya kwanza ya miezi mitano mfululizo (miezi 5
bila kuruka mwezi), na kufanya mambo haya manne kwa nia ya kumfariji Mama
Maria:
- Nenda
Kwenye Kitubio: (Ikiwa huwezi
kupata nafasi siku hiyo kwa sababu halali, toba ya dhati ya moyoni inatosha,
mradi una nia ya kwenda mara tu ukipata nafasi).
- Pokea
Komunyo Takatifu: (Kama una
ugonjwa au upo mbali na Kanisa, unaweza kufanya Komunyo ya Kiroho ukiwa
nyumbani).
- Sali
Rozari: Sali mafungu
matano ya Rozari (Rozari moja ya kawaida ya siku hiyo).
- Kaa
na Mama Maria kwa Dakika 15:
Hapa usisali Rosari. Kaa tu kwa utulivu kwa robo saa ukitafakari siri au
mafumbo ya Rosari. Ni kama umekaa unazungumza na mama yako wa karibu.
Ahadi ya Ajabu ya
Mama Maria
Ukiikamilisha ibada hii ya miezi mitano
kwa uaminifu, Mama Maria ametoa ahadi kubwa na ya kufariji sana:
Anahadi kukusaidia wakati wa saa yako
ya kufa kwa kukupa neema zote zinazohitajika ili uende Mbinguni (wokovu).
Hutakuwa peke yako siku hiyo ya mwisho.
Kitu cha Kukumbuka
Kila Siku: "CROSS"
Ili kufanya maisha yetu ya kiroho yawe
rahisi, tunaweza kukumbuka neno hili la Kiingereza C.R.O.S.S. (Msalaba):
- C
(Consecration) – Kujiweka Wakfu:
Kujikabidhi kwa Yesu kupitia Maria kila siku.
- R
(Rosary) – Rosari: Kusali Rosari
kila siku kwa ajili ya amani duniani.
- O
(Offer Up) – Kutoa Sadaka:
Kugeuza shida na kazi zako za kila siku kuwa sala.
- S
(Scapular) – Skapulari:
Kuvaa Skapulari ya Kahawia kama alama ya upendo wako kwake.
- S
(Saturdays) – Jumamosi:
Kutimiza Ibada hii ya Jumamosi ya Kwanza.
Kwa Nini Jambo Hili
ni Muhimu Leo?
Watu wengi wanalalamika kuwa ulimwengu
hauna amani. Lakini ukweli ni kwamba, wengi wetu hatujafanya upande wetu wa
kazi tumepuuza ibada hii rahisi ya Jumamosi Tano za Kwanza.
Mabadiliko ya ulimwengu hayaji kwa
kulalamika, yanakuja pale mimi na wewe tunapopiga magoti na kumfariji Mama yetu
wa Mbinguni.
Je, utaanza nami Jumamosi ya kwanza
inayokuja? Hebu tufanye hivi kwa pamoja!

0 Comments