Mara nyingi katika ukatoliki wetu kutokana na hali yetu ya mazoea tunashindwa kuthamini na kuelewa neema na ukuu wa Ekaristi takatifu hali inayopelekea kushindwa kuipa sakramenti hii heshima inayostahili. Basi karibu nitaeleza juu ya umuhimu wa sakramenti hii katika Maisha yetu ya kikristu.
Ni muhimu kukumbuka kuwa Ekaristi Takatifu ni chemichemi na kilele cha Maisha yote ya Kikristo, sakramenti nyingine zote zinatuandaa kupokea Ekaristi na zote zinaelekezwa kwake. Ekaristi Takatifu ni Mungu Pamoja nasi (Mathayo 1:23), katika Ekaristi Takatifu mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe. Katika Ekaristi Takatifu ni Kristu mwenyewe katika mwili,damu, Roho na Umungu wake.
Katika kuelezea Ekaristi Papa Pius XII alifundisha “Imani ya kanisa ni hii: neno la Mungu na Mwana wa Maria aliyeteseka msalabani,mtawala wa mbinguni, ni yeye yule yule katika Ekaristi”.
Bwana wetu Yesu Kristu alianzisha sakramenti hii kama chakula kutuonesha kuwa kile ambacho chakula cha kawaida hukifanya katika uzima wetu wa mwili, Komunyo takatifu hukitekeleza kwa namna ya ajabu katika uzima wetu wa kiroho. Sakramenti hii inatupatia uzima wa neema katika Roho zetu, tunahitaji Ekaristi takatifu ili kuwa na uzima ndani ya Roho zetu, kama vile chakula cha kawaida kinavyotupatia nguvu ya kuishi vivyo hivyo Ekaristi inaipa Roho nguvu mpya ya neema.
Kwa kadri ya mtaguso wa Trenti Ekaristi yatuosha dhidi ya dhambi zisizo za mauti na kutuepusha na dhambi za mauti. Sakramenti hii inatuunganisha na Kristo kwa sababu hiyo kutokana na Usafi na utakatifu wa Yesu tunayempokea tunaoshwa dhambi za zamani na tunakingwa na dhambi zijazo. Mt. Ambrose anasema “Kila tunapoipokea Komunyo twayatangaza mauti ya Bwana” Kama tunayatangaza mauti ya Bwana, tunatangaza ondoleo la dhambi. Kwa kuwa kila mara damu yake inapomwagika, humwagika kwa maondoleo ya dhambi, basi tunapaswa, siku zote kuipokea kusudi siku zote ituondolee dhambi zetu.
Kama nilivyosema mwanzo chakula cha mwili kinaturudishia nguvu zilizopotea vivyo hivyo, Ekaristi huimarisha mapendo ambayo, katika Maisha ya kila siku yalielekea kudhoofika, Kristu anahuisha mapendo yetu na hutuwezesha kuvunja kugandamana kwa ovyo na viumbe au mali zetu, na kutusaidia kujizamisha ndani yake.
Daima ni muhimu kukumbuka kuwa kama kweli tunataka kuacha Maisha ya dhambi hatuna budi kupokea Ekaristi kwani hutukinga tusitende dhambi za mauti. Kadri tunavyoshiriki uzima wa Kristo, na kadiri tunavyoendelea katika urafiki naye kwa sakramenti hii, ndivyo inakuwa vigumu zaidi kujitenga naye kwa dhambi za mauti. Hapa ni muhimu kukumbuka kuwa Ekaristi haipo kwa lengo la kuondoa dhambi za mauti.Kuondolea dhambi za mauti ni kazi kubwa hasa ya Sakramenti ya Kitubio (Upatanisho). Katekisimu ya kanisa Katoliki inaeleza kuwa “Ekaristi ni hasa sakramenti ya wale walio katika ushirika kamili na Kanisa” yaani katika hali ya neema, katika hali ya kutokuwa na dhambi ya mauti. Hivyo ni muhimu kukumbuka kutubu dhambi zote za mauti katika sakramenti ya kitubio, kabla ya kupokea Ekaristi Takatifu pale unapojua umetenda dhambi ya mauti.
"Ekaristi Takatifu ndio
barabara yangu kuelekea mbinguni." Haya ni maneno ya mwenye heri Carlo Acutis, mmoja wa
mashujaa wa Ekaristi katika siku za hivi karibuni, ambaye alifariki kutokana na
kansa ya damu(Leukemia) akiwa na umri wa miaka 15 mwaka 2006. Maisha
yake yote yalichochewa na Ekaristi Takatifu. Akionyesha hamu ya kutaka wengine
kumjua Bwana katika Ekaristi Takatifu kama yeye alivyofanya, alianzisha tovuti
(website) inayoorodhesha miujiza mbalimbali ya Ekaristi, ambayo bado ipo leo.
Na upendo wake kwa Ekaristi ulimiminika katika upendo halisi na huduma kwa
wengine, hasa kwa maskini, lakini pia karibu na nyumbani, kwa mwanafunzi
mwenzake aliyemfahamu aliyekuwa akikabiliana na hali ngumu ya familia.
Basi katika kuhitimisha ni
muhimu kujiuliza Je, Yesu katika Ekaristi ndiye kitovu cha maisha yako? Au
mambo mengine yanavamia kuchukua mahali pake? Je, Ekaristi inachukua nafasi ya
saa moja tu kila Jumapili kwako? Au Yesu kati yetu katika Ekaristi ndiyo
"barabara" yako, njia yako ya haraka kwenda mbinguni?
Ni kwa kuishi maisha yetu kila siku tukiwa na Ekaristi katikati ya Maisha yetu ndipo tutapata amani na utimilifu, nguvu na furaha. Lazima tuweze kuishi kwa kukiri kuwa , Yesu ndiye kila kitu katika Maisha yetu. Hali tulizonazo na marafiki tulionao wanaweza kubadilika. Lakini ni Mungu pamoja-nasi pekee hasa katika Sakramenti Takatifu ambaye ni thabiti. Basi tumfanye na awe kweli kitovu cha maisha yetu, kwa maana yeye pekee si wa kubadilishika. Na Ekaristi iwe kwetu, pia, "barabara yetu kuelekea mbinguni"!
0 Comments