Machapisho yanayopendwa

6/recent/ticker-posts

UJUMBE KUTOKA KWA MAMA YETU BIKIRA MARIA HUKO AKITA, JAPANI.

 

Bikira Maria

Matokeo ya Bikira Maria huko Akita, Japani, kwa Sr. Agnes Sasagawa.

Matukio ya ajabu yalianza tarehe 12 Juni 1973, siku hii Sr. Agnes aliona miale ya ajabu ya mwanga ikitokea ghafla kutoka kwenye Tabernakulo. Hali hiyo ilitokea tena siku mbili zilizofuata.

Mnamo tarehe 28 Juni 1973, kidonda chenye umbo la msalaba kilijitokeza mkono wa kushoto wa Sr. Agnes. Kilitokwa na damu nyingi na kumletea maumivu makali. Mnamo tarehe 6 Julai, Sr. Agnes alisikia sauti ikitoka kwenye sanamu ya Bikira Maria Mtakatifu ndani ya kanisa alipokuwa akisali. Sanamu hiyo ya Bikira Maria ilichongwa kutoka kwenye kipande kimoja cha mti wa Katsura na ina urefu wa futi tatu. Siku hiyo hiyo, baadhi ya masista waliona matone ya damu yakitiririka kutoka mkononi mwa sanamu hiyo ya Bikira Maria. Tukio hili la damu kutiririka lilijirudia mara nne. Kidonda kilichoonekana kikitoa damu katika sanamu hiyo kilibaki hadi tarehe 29 Septemba, ambapo kilipotea. Mnamo tarehe 29 Septemba, siku ambayo kidonda kwenye sanamu kilipotea, masista waliona sanamu hiyo ikianza kutokwa na jasho, hasa kwenye paji la uso na shingo. Mnamo tarehe 3 Agosti, Sr. Agnes alipokea ujumbe wa pili. Hatimaye mnamo tarehe 13 Oktoba 1973, alipokea ujumbe wa tatu na wa mwisho.

bikira maria


Miaka miwili baadaye, tarehe 4 Januari 1975, sanamu ya Bikira Maria ilianza kutoa machozi. Iliendelea kutoa machozi kwa vipindi kwa miaka 6 na miezi minane iliyofuata. Jumla sanamu hiyo Ilitoa machozi mara 101.

bikira maria

Ujumbe wa kwanza wa Bikira Maria  kwa Sr. Agnes Julai 6, 1973.

"Binti yangu, mtawa wangu, umenitii vizuri kwa kuacha yote kunifuata. Je, ugonjwa wa masikio yako unauma? Uziwi wako utapona, kuwa na uhakika. Je, kidonda cha mkono wako kinakuletea maumivu? Omba kwa ajili ya kulipia dhambi za watu. Kila mtu katika shirika hili ni binti yangu wa kipekee. Je, unasema vizuri sala ya Watumishi wa Ekaristi? Basi, tusali pamoja."

"Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliopo kweli katika Ekaristi Takatifu, nakutolea mwili wangu na nafsi yangu yote iunganishwe kabisa na Moyo Wako, moyo unaotolewa kila wakati katika altare zote za dunia na kumtukuza Baba kwa kuomba ujio wa Ufalme Wake.Tafadhali pokea toleo hili la unyenyekevu wa nafsi yangu. Nitumie kama utakavyo kwa utukufu wa Baba na wokovu wa roho.Mama Mtakatifu wa Mungu, usiniache nitengane na Mwanao wa Kimungu. Tafadhali nitete na kunilinda kama Mwanao Maalum. Amina."

Sala ilipomalizika, Sauti ya kimbingu ilisema:

"Sali sana kwa ajili ya Papa, Maaskofu, na Mapadre. Tangu Ubatizo wako umesali kwa uaminifu kwa ajili yao. Endelea kuomba sana...sana. Mwambie mkuu wako yote yaliyotokea leo na mtatii kwa kila atakayokuambia. Ameomba kwamba usali kwa bidii."

 Ujumbe wa pili wa Bikira Maria  kwa Sr. Agnes Agosti 3, 1973.

"Binti yangu, mtawa wangu, je, unampenda Bwana? Ikiwa unampenda Bwana, sikiliza ninachotaka kukuambia."

"Ni muhimu sana...Utamfikishia mkuu wako."

"Watu wengi ulimwenguni humtesa Bwana. Natamani roho zimpe faraja ili kupunguza hasira ya Baba wa Mbinguni. Nataka, pamoja na Mwanangu, roho ambazo zitafanya upatanisho kwa mateso yao na umaskini wao kwa ajili ya watenda dhambi na wale wasio na shukrani."

"Ili ulimwengu ujue hasira Yake, Baba wa Mbinguni anajiandaa kuleta adhabu kubwa kwa wanadamu wote. Mimi pamoja na Mwanangu nimeingilia mara nyingi ili kutuliza hasira ya Baba. Nimezuia kuja kwa maafa kwa kumtolea Mateso ya Mwanangu Msalabani, Damu Yake ya Thamani, na roho zilizochaguliwa zinazompa faraja kwa kuunda kikosi cha roho za sadaka. Sala, toba na matoleo ya ujasiri yote hayo yanaweza kupunguza hasira ya Baba. Nataka hili pia kutoka kwa shirika lako... kwamba shirika lako lipende umaskini, lijitakase na kuomba kwa ajili ya upatanisho wa dhambi na kukosa shukrani kwa watu wengi." 

"Sali sala ya Watumishi wa Ekaristi kwa ufahamu wa maana yake; itekeleze; toa upatanisho (chochote Mungu atakachotuma) kwa ajili ya dhambi. Kila mmoja ajitahidi, kulingana na uwezo na nafasi yake, kumtolea Bwana nafsi yake yote." 

"Hata katika taasisi ya kidunia sala ni muhimu. Tayari roho zinazotaka kuomba ziko njiani kuunganishwa. Bila kujali sana, kuwa waaminifu na wenye bidii katika sala ili kumfariji Bwana."

Baada ya ukimya Bikira Maria alisema:

"Je, unachofikiria moyoni mwako ni kweli? Je, umeamua kweli kuwa jiwe lililokataliwa? Mtawa wangu, wewe unayetaka kumilikiwa na Bwana bila kujiweka kando, kuwa mke anayestahili Mchumba, fanya nadhiri zako ukijua kwamba lazima uwekwe msalabani na kugongelewa misumari mitatu. Misumari hiyo mitatu ni umaskini, usafi, na utii. Kati ya yote, utii ndio msingi. Kwa kujiachilia kabisa, ruhusu uongozwe na mkuu wako. Atajua jinsi ya kukuelewa na kukuongoza." 

Ujumbe wa tatu wa Bikira Maria  kwa Sr. Agnes Oktoba 13, 1973.

"Binti yangu mpendwa, sikiliza vizuri ninachotaka kukuambia. Utamwambia mkuu wako."

Baada ya ukimya mfupi:

"Kama nilivyokuambia, ikiwa watu hawatatubu na kujirekebisha, Baba ataleta adhabu kubwa kwa wanadamu wote. Itakuwa adhabu kubwa kuliko gharika, ambayo haijawahi kuonekana hapo awali. Moto utaanguka kutoka mbinguni na kuangamiza sehemu kubwa ya wanadamu, wazuri na wabaya, bila kuacha mapadre wala waumini. Waliobaki watakuwa katika hali ya huzuni kiasi kwamba watatamani kufa tu. Silaha pekee zitakazobaki kwako zitakuwa ni Rozari na Ishara zilizoachwa kutoka kwa Mwanangu. Kila siku sali sala ya Rozari. Kwa Rozari, ombea Papa, maaskofu na mapadre."

"Kazi ya shetani itaingia hata ndani ya Kanisa kwa njia ambayo itasababisha makardinali kupingana na makardinali, maaskofu dhidi ya maaskofu. Mapadre wanaoniheshimu watadharauliwa na kupingwa na wenzao...makanisa na madhabahu yatavunjwa; Kanisa litajaa watu wanaokubali maafikiano na shetani atawashawishi mapadre na roho zilizotolewa kwa Mungu kuacha huduma ya Bwana." 

"Shetani atakuwa katili sana dhidi ya roho zilizotolewa kwa Mungu. Fikra ya kupoteza roho nyingi inasababisha huzuni yangu. Ikiwa dhambi zitaongezeka kwa idadi na uzito, hakutakuwa na msamaha tena kwao."

"Kwa ujasiri, zungumza na mkuu wako. Atajua jinsi ya kuhamasisha kila mmoja wenu kuomba na kutekeleza kazi za upatanisho."

"Ni Askofu Ito, anayesimamia shirika lenu."

Na Akatabasamu na kisha kusema:

"Bado una jambo la kuuliza? Leo ni mara ya mwisho nitakaponena nawe kwa sauti ya moja kwa moja. Kuanzia sasa utatii yule aliyetumwa kwako na mkuu wako."

"Sali sana sala ya Rozari. Mimi peke yangu bado naweza kukuokoa kutokana na maafa yanayokaribia. Wale wanaoamini kwangu wataokolewa."

Kifo cha Sr. Agnes Sasagawa.

bikira maria

Sista Agnes Sasagawa, Mtokewa wa Bikira Maria huko Akita Japan ambaye alipokea ujumbe wa Bikira Maria alifariki tarehe 15.08.2024, siku ambayo kanisa liliadhimisha Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni, alifariki akiwa na umri wa miaka 93.

 

Post a Comment

0 Comments