Isipokuwa
Ekaristi, hakuna sala inayopendwa zaidi duniani kote kuliko Rozari takatifu. Je, ni ipi historia ya rozari, sala hii
ilitokea wapi na kwa nini inaendelea
kuwa maarufu katika mipaka mingi, tamaduni, na nyakati? Historia ya Rozari
inajaa ukweli, hadithi, mithali, na utakatifu wa kweli. Kwa zaidi ya miaka 600,
Rozari imekuwa ni alama ya maisha ya kiroho ya Kanisa Katoliki na imekuwa ni njia inayovutia sana ya sala kwa mamilioni
ya watu wengi.
Asili
ya Rozari inatokana na vyanzo viwili tofauti: chanzo cha kwanza kina miaka 3000
na kinapatikana katika zaburi zinazomhusu Mfalme Daudi katika Maandiko ya
Kiebrania ya Agano la Kale; cha pili ni mazoea ya kuhesabu sala kwa kutumia
lulu, mawe, au alama kwenye mbao au jiwe. Mazoea haya, yanayopatikana katika
dini kubwa duniani kama wahindu, wabudha, Taoism, na Uislamu, ni ya zamani sana
pia.
Zaburi
zinazofikia 150 zinatoka katika maandishi ya Kiebrania ya mapema karibu na
wakati wa Wafalme Daudi na Solomoni. Wayahudi walikuwa wakisali zaburi hizo
wakati wa Yesu, na hata Yesu mwenyewe
aliomba na kuzinukuu hata msalabani alipokuwa anakufa: "Eloi, Eloi, lama
sabachthani?" (Zaburi 22).
Wamonaki
Wakristo wa mapema waliokimbia jangwani
kuepuka machafuko ya dunia na kutafuta Mungu na utakatifu walikuwa wakisali
zaburi hizo kwa seti za 50. Walifikiria kwamba walikuwa wakisali pamoja na
Mfalme Daudi na manabii na watakatifu wa zamani na pia pamoja na Yesu. Walianza
haraka kusali zaburi hizo pamoja kama jumuiya na kutumia mapande ya papirusi au
ngozi ya kondoo kusoma. Wengi wa hao monaki hawakuweza kusoma au kuelewa
Kilatini, ambayo ilikuwa ni lugha ya Biblia katika Karne ya Kati.
Watu wengi nje ya monasteri hawakuwa na mapande au vitabu na pia hawakuwahi kujifunza kusoma na kuandika. Hata hivyo, monaki wasiojua kusoma waliokuwa wakifanya kazi shambani, na waumini wengi wa dhati walitaka kushiriki katika maisha ya sala za Kimonaki waliojua kusoma na wa Kanisa. Kwa kuwa hawakujua Kilatini na hawakuweza kukumbuka zaburi zote 150, hatua kwa hatua walianza kuzibadilisha kwa kusali sala ya Paternosters yaani sala ya Baba Yetu. Walihitaji njia ya kuhesabu sala walizosali, kwa hivyo waliweka sala hizo kwenye vikundi vya 50, kama ilivyokuwa kwenye Zaburi. Bado walihitaji njia ya kuhesabu, hivyo waliweka vijiti vidogo au vitu vingine, ambavyo baadaye viligeuka kuwa punje, sawa na vile vilivyotumika katika dini nyingine kuhesabu sala na vitendo vya ibada.
Kuna
hadithi nzuri ya mmonaki aliyeitwa Paulo wa Misri katikati ya karne ya 4
aliyekuwa akikusanya mawe 300 na alikuwa akitupa mawe hayo kila alipomaliza
kusali sala. Kadri alivyosali, ndivyo alivyokuwa mwepesi. Hadithi hii ina
uwezekano mkubwa wa kuwa ya kufikirika. Hapa tunaweza kuona muungano wa vyanzo
viwili vya Rozari: Zaburi za Kiebrania za Daudi na kuhesabu punje kutoka kwa enzi za kabla ya Ukristo.
Hadithi
nyingine inayodhaniwa kuwa kweli hadi karne ya 19 na 20 ni kuhusu tokeo la Bikira Maria kwa Mtakatifu Dominiko
mwaka wa 1208 kumpatia Rozari kama tunavyojua leo. Kulingana na hadithi hii,
Bikira Maria alimtia moyo Dominiko na Wadominiko kusambaza ibada kwake yeye na
Mwana wake kupitia Rozari, akihakikisha kuwa neema nyingi zingewafaidi wote
waliokuwa wakisali Rozari.
Hata
hivyo, kulingana na Padre Richard Gribble, C.S.C., ni hadi karne ya 15 ambapo
Rozari ilianza kuchukua umbo tunalolijua leo. Katika kipindi hiki, mafumbo na
sala binafsi zilianza kuungana. "Baba Yetu" ilikuja moja kwa moja
kutoka Injili ya Mathayo, sura ya 6. Sehemu kubwa ya sala ya "Salamu Maria" pia ilitoka kwenye
Maandiko, kwa kuunganisha salamu mbili: kwanza kutoka kwa Malaika Gabrieli
kwenye Habari Njema na pili kutoka kwa Binamu wa Maria, Elizabeti, katika Kumtembelea
kutoka Injili ya Luka. "Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi
wakosefu sasa na saa ya kufa kwetu. AMINA" imetoka kwenye sala maarufu ya
waumini wakati huo.
Kanuni
ya Mitume, inayofuatia Ishara ya Msalaba, ni ya zamani. Marejeo ya mapema ya neno "Kanuni ya Mitume"
yanapatikana katika barua ya Mtakatifu Ambrosio ya mwaka wa 390 kutoka kwenye
sinodi Iliyofanyika huko Milano. Kanuni ya Mitume inaweza kuwa imehusishwa na
imani, iliyokubaliwa sana katika karne ya nne, kwamba, chini ya uongozi wa Roho
Mtakatifu, kila mmoja wa Mitume Kumi na Wawili alitoa kifungu chake kati ya
vipande kumi na viwili vya Kanuni. Ingawa haikuwa katika sura yake ya sasa hadi
mwaka wa 341 BK, Kanuni ya Mitume inaakisi kwa uaminifu mafundisho
waliyoyapeleka Roma na sehemu nyingine ya dunia inayojulikana.
Salve
Regina yaani Salamu, Malkia Mtakatifu imeanza
kutumika kutoka karne ya 11 na mara
nyingi inasaliwa mwishoni mwa kusali Rozari. Ingawa sala hizi zilikuwa maarufu
kwa miaka 300, hazikuwekwa katika sura yake ya mwisho tunayojua hadi Mtaguso wa
Trento, 1545-1563.
0 Comments