Machapisho yanayopendwa

6/recent/ticker-posts

BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI.

 

Kwa ajili ya kuwa Mama wa mkombozi Maria alitajirishwa na Mungu kwa Karama nyingi zenye kulingana na kazi hiyo kubwa ya kumzaa mkombozi wa Ulimwengu.

Karne kwa karne kanisa limetambua kwamba Maria aliyejazwa neema na Mungu, alikombolewa tangu mwanzo kwa kuchukuliwa kwake  mimba. Ndicho yanachofundisha mafundisho ya Imani juu ya kukingiwa dhambi ya asili yaliyotangazwa na Papa Pius IX alipokiri kuwa fundisho hili la kukingiwa dhambi ya asili kuwa ni Dogma katika Waraka wake uitwao Ineffabilis Deus, uliotolewa 8 Desemba mwaka 1854 alisema:

“Mwenye heri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema ya upendeleo wa pekee wa Mungu mwenyezi, kwa kutazamia mastahili ya Yesu Kristo, mwokozi wa Wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi  ya asili”.

Bikira Maria kama wanadamu wengine alihitaji kukombolewa dhidi ya dhambi,  naye alikombolewa dhidi ya dhambi  kwa kutazamia mastahili ya mwanae, kama  anavyokiri yeye mwenyewe katika utenzi wake kwa kusema “Roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu” Luka 1:47.

 Kila mwanadamu isipokuwa Bikira Maria wote alikombolewa kutoka katika dhambi na upotevu wa milele kupitia mateso na kifo cha Yesu msalabani. Lakini Mama Bikira Maria yeye alikingwa kabisa dhidi ya dhambi, na dhidi ya kutenda dhambi.

Ili kuelewa tofauti ya aina hizi mbili za ukombozi dhidi ya dhambi, fikiria mfano umepigwa risasi na akaja mtu akakusaidia kuondoa risasi ile na kuponya Donda lako, hakika utamuita mtu huyo mkombozi wako. Pia fikiria iwapo wakati unataka kupigwa risasi kabla ya risasi hiyo haijakufikia akaja mtu akakuepusha dhidi ya risasi hiyo. Hawa wote utawaita wakombozi wako lakini kwa namna tofauti. Wa kwanza amekukomboa baada ya kupigwa risasi na wapili ni kabla ya kupigwa risasi. Hivi ndivyo ilivyo hata katika ukombozi wetu na ule wa Bikira Maria.

Zaidi ya mtu yeyote yule aliyeumbwa, Mungu Baba alimbariki Bikira Maria kwa baraka zote za Rohoni, katika ulimwengu wa Roho, ndani yake Kristo na akamchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili awe mtakatifu na bila hatia  mbele zake katika pendo ili astahili kumbeba mwanae wa pekee yaani Yesu Kristo, aliyemtakatifu sana, Mungu Baba asingeweza kuruhusu mwanae akae sehemu yenye dhambi. Kwa neema ya Mungu Mama Maria amebaki safi kabisa na hakutenda dhambi yoyote Maisha yake yote.

Post a Comment

0 Comments