Machapisho yanayopendwa

6/recent/ticker-posts

NOVENA YA HURUMA YA MUNGU SIKU YA TISA


 

Maneno ya Mwokozi: “Leo niletee roho za wale waliokwishaingia hali ya uvuguvugu, na uwazamishe katika kilindi cha Huruma yangu. Roho hizi huumiza sana Moyo wangu. Roho yangu iliteseka sana kwa kinyaa cha kutisha kule bustanini kwa sababu ya roho hizi vuguvugu. Ni wao waliosababisha nilie; Baba ikiwa ni mapenzi yako uniondolee mbali kikombe hiki nisikinywe. Kwa watu hawa, tumaini la mwisho lililowabakia ni kuikimbilia Huruma yangu tu basi”.

Kiongozi: Tuwaombee watu walio na hali ya uvuguvugu, hali ya hatari kwa wokovu, ambao walisababisha mateso makali sana kwa Yesu Kristu kule bustanini mwa mizeituni.

Ee Yesu mwenye Huruma nyingi, Wewe u Huruma yenyewe, Uzipokee roho vuguvugu ndani ya Moyo wako ulio na Huruma bila kiasi. Roho hizi ni kama mizoga iliyojaa na kunuka uvundo, uziingize katika moto wa upendo wako safi, zitakasike. Roho hizi zilikutia kinyaa kingi. Sasa uziwashe tena, na kwa Huruma yako, uzipe paji la Upendo Mtakatifu. Ee Yesu mwenye Huruma Kuu, tumia uwezo wako na uzipatie roho hizi bidii tena, kwani kwako hakuna kitu kisichowezekana, na kwa njia hii wapate kuitukuza daima Huruma Yako. Amina

Baba yetu... Salamu Maria … Atukuzwe...

Baba wa Huruma, uzitazame kwa macho ya Huruma, roho zilizo vuguvugu, ambazo katika hali yao hiyo, wameingizwa ndani ya Moyo wa Mwanao Yesu, ulio kilindi cha Huruma. Ee Baba wa Huruma, tunakusihi kwa ajili ya mateso makali ya Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, uliyovumilia pale msalabani, kwa masaa matatu ukiwa katika hali ya umahututi ya uchungu, uziwezeshe hata roho hizi zipupie utukufu wako. Uijaze mioyo ya watu hawa upendo wa kweli, hivyo kwa Baraka takatifu, waweze kutenda matendo mengi ya huruma hapa duniani, na huko Mbinguni wafike kuitukuza Huruma yako Kuu kwa milele yote. Amina


Post a Comment

0 Comments