Picha hii ilifunuliwa katika maono yake Mt. Faustina tarehe 22.02.1931, akiwa chumbani kwake katika nyumba ya watawa huko Plock. Alisema “Jioni nikiwa chumbani kwangu, nilimuona Yesu akiwa katika mavazi meupe. Mkono wake mmoja uliinuliwa katika ishara ya kubariki, mmoja ulikuwa umeshika vazi lake kifuani. Katika vazi lake chini kidogo ya kifua chake ilitoka miale mikubwa miwili ya mwanga, mmoja mwekundu, mwingine kama maji… baada ya muda kidogo , Yesu aliniambia ‘chora picha kama unavyoiona hapa na chini ya picha hiyo uandike maneno haya: Yesu Ninakutumaini! Naahidi kwamba Roho yeyote itakayotukuza picha hii haitaangamia kamwe. Naahidi pia ushindi kwa maadui wa roho hiyo walio duniani humu, hasa saa ya kifo chake. Mimi mwenyewe nitailinda kama utukufu Wangu’” (shajara ya Mt. Faustina, 47,48).
Bwana Yesu alipoulizwa maana ya miale miwili ya mwanga alisema “miale hiyo miwili inamaanisha Damu na maji. Miale ya maji ni kwa ajili ya yale Maji yatakasayo Roho na kuzifanya zenye haki; miale mwekundu humaanisha damu ambayo ni uzima wa Roho… Heri atakayefunikwa na miale hiyo, mkono wa Mungu wa haki hautamgusa.” (Shajara ya Mt.Faustina 299). Sakramenti za kitubio na Ubatizo, zinasafisha Roho, Ekaristi inastawisha Roho. Basi miale hii miwili inaonesha Sakramenti takatifu na neema zote za Roho Mtakatifu.
Picha ya Yesu wa Huruma inafaamika kama “Picha ya huruma ya Mungu”.Picha hii sio tu inaonesha huruma ya Mungu bali ni ishara ya kuwakumbusha wakristu juu ya wajibu wa kumtumainia Mungu na kuwa na upendo hai kwa Jirani.
0 Comments