Kabla
ya kupata mwenzi wa kungia nae katika mahusiano nae pengine kuishi pamoja nae katika
ndoa takatifu, hakika kila mmoja anakuwa tayari na vigezo au sifa fulani anazotamani
kuziona kwa mwenzi wake; mtu anakuwa na yale anayoyapenda na asiyoyapenda,
baadhi ya watu watakuwa na sifa hizo na wengine watakosa sifa hizo.
Mungu
pia wakati wa uumbaji wake tayari alikuwa na namna alivyotaka ulimwengu
uonekane, kama ilivyokawaida kabla ya kujenga nyumba mjenzi anahitaji ramani ya
nyumba ili kutekeleza ujenzi wa nyumba vizuri. Kila kitu kilichopo duniani hapa
kilikuwepo katika akili ya Mungu tangu milele yote.
Mungu
alipomuumba mwanadamu alikuwa na mawazo mawili juu ya mwanadamu kwanza ni vile
atakavyokuwa mwanadamu yaani umbile lake na pili ni vile atakavyo takiwa
kuishi. Lakini mwanadamu hakuweza kuishi vile alivyotakiwa kuishi, aliishi
kinyume na mpango wa Mungu juu yake.
Mwanadamu
mmoja tu ndiye aliyeishi kwa asilimia mia moja, yaani aliishi kikamilifu kwa
kadri ya mpango wa Mungu juu ya kila mwanadamu, mwanadamu huyu si mwingine bali
ni Bikira Maria. Mawazo ya Mungu juu ya Maria yalikuwa sawasawa na jinsi
Maria alivyoishi hapa duniani.
Kwa
kuwa yeye ndiye vile ambavyo Mungu alitaka sisi sote tuwe, Maria ni mfano wa
milele akilini mwa Mungu, yule ambaye Mungu alimpenda hata kabla ya kuumbwa kwake.
Maria alikuwa pamoja na Mungu si tu wakati wa uumbaji, bali hata kabla ya
uumbaji. Yeye alikuwepo katika akili ya Mungu ata kabla ya kuwepo kwa mama
yeyote. Yeye ndiye Mama wa Mama wote duniani.
Mungu
si tu alimfikiria katika milele yote, bali pia alimfikiria mwanzoni mwa wakati,
mwanzo wa historia ya mwanadamu, wakati binadamu walipoanguka kwa kushawishiwa
na mwanamke, Mungu alimwambia shetani “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo
mwanamke, na kati ya uzao wako na wake, huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda
kisigino” (Mwanzo 3:15). Mwanamke anayezungumziwa hapa ni Bikira Maria sio
Eva, kwa kuwa Eva tayari alikubali kuwa chini ya shetani kumuasi Mungu
asingeweza kuwa adui wa shetani. Ni kama Mungu alikuwa akisema ikiwa ni kwa
mwanamke wanadamu walianguka, basi ingekuwa kwa njia ya mwanamke ambayo
angelipiza kisasi kwa shetani.
Yeyote
ambaye angekuwa Mama wa Mungu, bila shaka angebarikiwa kati ya wanadamu wote,
na kwa sababu Mungu mwenyewe alimchagua, angehakikisha kuwa vizazi vyote
vinamwita mbarikiwa.
0 Comments