Katika
Maisha ya mwanadamu kuna nyakati tunatenda dhambi nyingi sana, mara nyingi
katika hali hii tunakosa matumaini na kujiona kama tayari tumepotea hatuwezi
kuokolewa tena, kwa sababu tunaamini dhambi zetu ni kubwa sana kuliko huruma ya
mwenyezi Mungu, hali hii hupelekea kuishi katika Maisha ya kukata tamaa,
kujichukia na huzuni kila mara. Hali hii inatufanya wakati mwingine kuogopa
hata Kwenda kuungama dhambi zetu. Basi mpendwa usikate tamaa kabisa nafahamu
unaweza kuwa upo katika hali hiyo ya dhambi pengine ni ndugu au rafiki wa
karibu anapitia katika hali hii. Katika nyakati hizo tunauhitaji wa msaada
kutusaidia kutupa ujasiri wa Kwenda kufanya maungamo ili kurudi tena kuwa Mwana
wa Mungu. Mama Maria atakuwa msaada mkubwa katika hali hii kwani yeye ni
kimbilio la wakosefu.
Bikira
Maria alimtokea Mt. Brigita na kumweleza kuwa, Yeye (Bikira Maria) sio tu mama
wa wenye haki na wasio na hatia bali pia ni Mama wa wadhambi wanaotaka kutubu
dhambi zao. Katika hali ya dhambi Maria kama mama yetu anatupokea anatukumbatia
na kutusaidia kurudi kwa Mungu.
Katika
kitabu cha mwanzo tunaona “Mungu aliumba mianga miwili mikubwa, mkubwa
utawale mchana na ule mdogo utawale usiku” Mwanzo 1:16. Mwanga mkubwa ni
jua na mwanga mdogo ni mwezi. Mababa wengi wanaeleza kuwa Mwanga mkubwa
unamuakilisha Kristo anayetawala juu ya wenye haki na ule mdogo unamwakilisha
Mama Maria anayewaangaza wale waishio katika giza nene la dhambi. Kwahiyo mama
Maria anatuandaa katika giza la dhambi zetu, anatuandaa vema kabisa ili
kunapokucha tuweze kuwa tayari kuupokea Mwanga wa Kristo atawalaye wenye
haki. Katika kueleza hili Papa Innocent
III aliandika kwa kusema “yeyote aliyekatika usiku wa dhambi, basi aelekeze
macho yake kwa mwezi na kumuita Maria”. Tunapotenda dhambi tunapoteza neema ya mwanga wa haki, basi tumkimbilie
Mama Maria.
Ndugu
yangu ni muhimu kukumbuka kuwa Bikira Maria ni kama Safina la Nuhu ambalo ndani
yake waliingia kila aina ya Wanyama ili kupata ulinzi dhidi ya gharika ya
Mungu, basi ni katika kivuli hiki Mama Maria naye ni kama Safina anapokea na
kuwalinda wadhambi wote wa kila aina dhidi ya adhabu ya Mungu.
Kwa
kumkimbilia mama Bikira Maria utapata neema ya kutubu dhambi zako na kuziacha
kabisa. Mkimbilie mama huyu pale unapoanguka, Mama huyu ni mama bora kamwe
hamchoki mtu kwani sisi ni wanae, daima yupo tayari kutusaidia katika nyakati
zetu za shida hasa dhambi.
Unapotokea
umetenda dhambi mkimbilie, Sali kwake hasa Rozari Takatifu muombe akupe neema
ya kuacha dhambi na kupata nguvu ya Kwenda kuungama, tunahitaji neema ili
kukubali kukiri dhambi zetu kwa sababu kwa asili tendo la kuungama linahitaji
ujasiri mkubwa, basi Mama Maria kwake utapata ujasiri na neema ya kuacha dhambi
kupitia maombezi yake.
Daima
unapokuwa katika hali ya dhambi kumbuka maneno haya ya Bikira Maria kwa Mtakatifu Brigita “haijalishi ni dhambi
kiasi gani mtu ametenda, daima nipo tayari kupokea haraka mtu huyo....
siangalii wingi wa dhambi alizonazo, bali nia yake ya kutubu, sisiti kumbariki
na kuponya madonda ya dhambi, kwani ninaitwa na ni ndivyo ilivyo , MAMA WA
HURUMA”.
0 Comments