Machapisho yanayopendwa

6/recent/ticker-posts

HISTORIA YA ROZARI YA HURUMA YA MUNGU



Rozari hii ilitolewa na Yesu mwenyewe kwa sista Faustina huko Vilnius tarehe 13-14. Septemba 1935 kama sala ya malipizi ya dhambi zetu.

Mtakatifu Faustina alipata maono ya Malaika wa Bwana aliyetumwa kuangamiza mji Fulani. Sista Faustina alianza kuomba huruma lakini sala zake hazikuwa na nguvu yoyote. Ghafla hakaona Utatu Mtakatifu na nguvu ya neema ikamjia. Wakati huo alijikuta anamuomba Mungu huruma yake kwa maneno aliyoyasikia ndani ya moyo wake “Baba wa milele ninakutolea Mwili na damu, Roho na Umungu wa Mwanao mpenzi, bwana wetu Yesu Kristo, kwa kulipia dhambi zetu na dhambi za dunia nzima, kwa ajili ya mateso makali sana ya Yesu utuhurumie sisi na dunia nzima” Alipokuwa akiendelea kusali sala hii, Malaika alionekana kushindwa kutimiza adhabu hiyo (Shajara, 474,475 na 476).

Asubuhi ya siku iliyofuata  aliingia kanisani alisikia tena moyoni mwake sauti ikisema hivi; “kila mara unapoingia kanisani Sali sala niliyokufundisha jana.. sala hii itatuliza adhabu yangu. Utaisali kwa siku tisa katika punje za rozari kama ifuatavyo : kwanza utasali BABA YETU na SALAMU MARIA na KANUNI YA IMANI. Kisha katika punje za Baba Yetu utasema maneno yafuatayo “ “Baba wa milele ninakutolea Mwili na damu, Roho na Umungu wa Mwanao mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristo” na kwenye punje za Salamu Maria utasema maneno yafuatayo; “kwa ajili ya mateso makali sana ya Yesu utuhurumie sisi na dunia nzima”. Kwa kuhitimisha utasali mara tatu; “ Mungu Mtakatifu, mtakatifu mwenye enzi, mtakatifu usiyeweza kufa, utuhurumie sisi na dunia nzima”.

Tangu siku hiyo aliendelea kusali sala hiyo bila kukoma, akitoa hasa kwa ajili ya wanaokufa. Katika mafunuo mengine, Yesu alimdhihirishia kuwa Rozari hiyo haikuwa yake hasa, bali ilikusudiwa kwa ajili ya dunia nzima. Alitoa pia ahadi zisizo za kawaida kwa wale watakaoisali: “uwatie watu moyo ili wasali rozari hii niliyokupatia”. (shajara 1541) “yeyote akayeisali atapata huruma kuu saa ya kufa”(shajara 687) “watakaposali Rozari hii mbele ya mtu anayekufa, nitasimama kati ya Baba yangu na mtu huyo, si kama hakimu mwenye haki, bali kama MWOKOZI mwenye huruma” (shajara 1541). “ mapadre wawatolee wadhambi sala hii kama matumaini yao ya mwisho na wawafundishe hivyo. Hata mtu angekuwa na dhambi nyingiau Roho ngumu kiasi gani, asalipo rozari hii hata mara moja  tu, atapata neema zangu zisizo na mipaka”(shajara 687). “rozari hii itakupatia kila kitu, iwapo maombi yako hayatapingana na mapenzi yangu”. (Shajara 1731).

Rozari hii inaposaliwa kwa kutumia Rozari ya kawaida, Rozari ya huruma ya Mungu ni sala ya maombezi yenye nguvu ya kuongeza ukuu wa sadaka ya Ekaristi, hivyo inafaa isaliwe  baada ya mtu kuwa amepokea komunyo takatifu kwenye Misa takatifu. Inaweza kusaliwa muda wowote, lakini Bwana wetu alimwambia mtakatifu Sista Faustina  kuisali siku tisa kabla ya Sikukuu ya Huruma ya Mungu. Na alisema; “ kwa novena hii nitazipatia Roho neem azote zinazowezekana” (Shajara, 796).

Wataalamu wengi wa teolojia na ujumbe wa huruma ya Mungu wanasema mwamini anayesali kwa uchaji Rozari ya huruma anatimiza ukuhani wa Mkristo utokanao na ubatizo wake na kimsingi anatenda yale atendayo kuhani altareni anapogeuza  mkate na divai kuwa mwili wa bwana na damu yake ya thamani. Si kwamba, mkristo ana uwezo wa kutenda mageuzo kama padre wakati wa misa, lakini kwa kusali rozari  ya huruma anatimiza kikamilifu Ukuhani wake utokanao na ubatizo wake na kumtolea Mungu mwenye huruma sadaka ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyoitoa msalabani siku ya ijumaa kuu.

x

Post a Comment

0 Comments