Mtakatifu Maria Faustina Kowalska, anafahamika leo
kama “Mtume wa Huruma ya Mungu”.
Alizaliwa kama mtoto wa tatu katika familia ya Watoto
kumi, familia yake ilikuwa maskini na waliishi huko katika Kijiji cha
Glogowiec, kilichopo nchini Polandi. Alibatizwa katika kanisa la Parokia ya karibu iliyokuwa Swinice na
alipewa jina la “Helena”. Tangu
alipokuwa mdogo alikuwa tofauti na wenzake kwani alikuwa ni mcha Mungu,
alipenda sala, mwenye kujituma na mtii, aidha alikuwa ni mwenye huruma sana kwa
watu waliokuwa wakiteseka na taabu mbalimbali. Alisoma kwa muda wa miaka
mitatu, na alipofikisha umri wa miaka kumi nne kutokana na hali duni ya familia
yao aliondoka katika makazi ya familia yao na kuamua kutafuta kazi ili kusaidia
familia yake, na alifanya kazi za ndani katika miji ya karibu na kwao ya
Aleksandrow na Lodz.
Alipokuwa na umri wa miaka saba (miaka miwili kabla ya
kupokea komunio), Helena tayari alihisi katika Roho yake wito wa kuingia katika
Maisha ya kitawa. Alipowaeleza wazazi wake juu ya wito wake huo wazazi wake
walimkatalia. Kwa sababu ya kukataliwa alijitahidi kuzuia wito huu wa kimungu
uliokuwa ndani yake. Baada ya siku nyingi kupita siku moja alipewa maono ya Yesu akiwa anateseka na alimsikia
Kristu akimwambia “nitaendelea kukaa na wewe mpaka lini na wewe utaendelea
kuniacha mpaka lini”, baada ya maono
hayo alianza kutafuta nyumba ya masista(conventi) ambayo angejiunga nao.
Alikwenda katika nyumba nyingi za kitawa lakini sehemu zote alikataliwa. Hatimaye
tarehe 01.Agosti. 1925, alikubaliwa akaanza kukaa katika nyumba ya watawa wa
Bibi yetu wa Huruma iliyokuwa katika mtaa wa Zytnia huko Warsaw. Katika kitabu
cha Maisha yake aliandika hivi “ilionekana kwangu kama nimeingia katika
Maisha ya Paradiso. Sala moja ilikuwa ikitoka moyoni mwangu nayo ilikuwa sala
ya shukrani”.
Baada ya wiki chache kupita alipitia kishwawishi
kikubwa cha kutaka kuhama Kwenda katika nyumba ya shirika jingine la kitawa
ambapo alitamani kuwa angepata muda mwingi wa kusali. Akiwa katika hali hiyo
Bwana wetu alimtokea, alioneshwa uso wa Yesu ulioteswa, na Bwana alimwambia “ni
wewe utakaye sababisha maumivu haya kwangu utakapoondoka katika conventi hii.
Mimi nimekuita katika conventi hii na sio sehemu nyingine, na katika sehemu hii
nimekuandalia neema nyingi sana kwa ajili yako”.
Alipojiunga na masista hao alipewa jina la Sista Maria
Faustina. Alifanya unovisi wake huko Cracow,
huko Cracow Askofu Stanslaus Rospond, alimpa nadhiri zake za kwanza,
miaka mitano baadae aliweka nadhiri zake za daima za Usafi wa moyo, umaskini na
utii. Alipewa kazi katika nyumba zao za kitawa, lakini hasa huko Cracow, Plock
na Vilnius, alifanya kazi za kupika, kutunza bustani na kukaa getini.
Kwa mwonekano wake wa nje hakuna kitu chochote
kilichoonekana cha ziada. Alifanya kazi zake, alifuata sheria zote za kitawa,
alikuwa mtulivu na mwenye kukaa kimya, alikuwa mchangamfu siku zote, alijaa
ukarimu na upendo usio wa kibinafsi kwa Jirani.
Maisha yake yote yalihusisha kutafuta ukamilifu wa
muungano wa kweli kwa Mungu, kujitoa binafsi katika kushirikiana na Yesu katika
kazi ya kuokoa Roho. Katika kitabu cha Maisha yake aliandika “unajua toka
mwanzo wangu nimekuwa nikitaka kuwa mtakatifu mkubwa, yani hii inamaanisha
nimekuwa nikitaka kukupenda wewe kwa upendo mkubwa ambao hakuna Roho umewahi
kukupenda hivyo”.
Ni katika kitabu chake cha “Diary” yaani “Shajara”
ambacho kinatufunulia kina cha Maisha yake ya kiroho. Unaposoma kwa makini
kitabu cha Maisha yake kinatoa picha ya kilele kikubwa cha umoja uliokuwepo
baina ya Roho yake na Mungu, uwepo wa karibu sana wa Mungu kwa Roho yake,
Pamoja na jitihada zake na magumu yake katika njia ya kuuutafuta ukamilifu wa
kikristo. Bwana alimpa neema kubwa sana neema ya kutafakari, kwa ufahamu wa
kina sana mafumbo ya huruma ya Mungu,
kwa maono, ufunuo, madonda yaliyofichika, alipewa zawadi ya unabii na kuelewa
Roho za watu.
Maisha magumu na Maisha ya kufunga aliyoakuwa akiishi
hata kabla ya kujiunga na shirika lake la kitawa, yaliudhoofisha sana mwili
wake kiasi kwamba wakati akiwa mpostulanti alitakiwa apelekwe huko Skolimow karibu na Warsaw ili kuweka afya
yake sawa. Mwishoni mwa mwaka wake wa kwanza wa unovisi, alipatwa na maumivu
yasiyo ya kawaida ya ajabu yafahamikayo kama “Usiku wa giza” (Dark night), na
baadae alipata mateso kiroho yaliyohusiana na kukamilisha kazi yake aliyokuwa
akipewa na Kristo Bwana. Mt. Faustina aliyatoa Maisha yake sadaka kwa ajili ya
wadhambi na kwa sababu hii alipitia mateso makubwa sana, ili kuokoa Roho
mbalimbali za watu. Miaka yake ya mwisho wa Maisha yake alipitia mateso ya ndani ya mwilin na Roho yaliongezeka
sana. Aliugua ugonjwa wa Kifua kikuu ulioshambulia mapafu yake na mfumo wake wa
mmengenyo wa chakula. Kwa sababu hii alipelekwa hospitali kwa miezi kadhaa ili
kutibiwa huko katika mtaa wa Pradnik jijini Cracow.
Akiwa amedhoofika sana kimwili lakini amekomaa kiroho
alifariki na kuugana na Mungu tarehe 05. Oktoba.1938, akiwa na umri wa miaka
33, na alikuwa mtawa kwa muda wa miaka 13. Mwili wake ulizikwa katikaa makaburi
ya watawa huko Cracow-Lagiewniki. Na mwaka 1966, mwili wake uliamishwa wakati
wa hatua za kutangazwa kwake mtakatifu na uliwekwa katika kikanisa cha masista.
Kwa mwanamke huyu wa kawaida asiyekuwa msomi, lakini
mtawa jasiri, aliyemwamini bwana wetu
bila kikomo, Bwana wetu alimpa kazi kubwa ya kutangaza ujume wake wa Huruma kwa
ulimwengu wote, alimwambia “Leo ninakutuma
kwa huruma kwa watu wa ulimwengu
wote. Sitaki kuadhibu wanadamu, lakini ninatamani kuwaponya, kuwaweka katika
moyo wangu wa huruma” (Shajara, 1588) “Wewe ni karani wa huruma yangu,
nimekuchagua wewe kwa kazi hiyo katika Maisha haya na yale yajayo”(Shajara,
1605).
0 Comments