Machapisho yanayopendwa

6/recent/ticker-posts

Ibada ya Bikira Maria, Rosa Mystica

"Rosa Mystica" ni maneno ya Kilatini yenye maana ya "Waridi lenye fumbo." Jina hili mara nyingi linahusishwa na Bikira Maria katika tamaduni ya Kikatoliki. Linawakilisha usafi, uzuri, na asili yake ya kiroho. Maneno haya hutumiwa mara kwa mara katika sala na nyimbo zilizoandikwa kwa heshima ya Maria

Ibada kwa Bikira Maria  kwa jina la  "Rosa Mystica" ni tamaduni ya kale katika Kanisa, ambapo ubora wa pekee wa Mama Yetu uliwakilishwa kishairi kwa uzuri na harufu nzuri ya waridi, maua yanayochukuliwa kuwa ndiyo maua bora zaidi.

Ibada hii  kwa Bikira Maria Rosa Mystica ilitiwa nguvu katika nyakati hizi za sasa baada ya Bikira Maria kutokea  huko Montichiari na Fontanelle, nchini Italia.

Huko Italia Bikira Maria alimtokea  muuguzi aitwaye Pierina Gilli - kuanzia mwaka 1947, na matokeo hayo ya Bikira maria yaliendelea hadi muda mfupi kabla ya kifo cha muuguzi huyo mwaka 1991.

Bikira Mtakatifu alijitambulisha mwenyewe kama "Maria, Rosa Mystica, Mama wa Kanisa" na kutoa ujumbe muhimu hasa kwa makuhani na watawa. Aliwahimiza waishi miito yao kwa heshima, huku akiwataka wale walio katika miito mingine kuwaombea

"Mimi ni Mama wa Yesu na Mama wa nyote. Bwana wetu amenituma kuwaletea ibada mpya ya Maria kwa taasisi zote za kiume na kike, mashirika ya kidini, na makuhani wote. Ninaahidi taasisi hizo za kidini, mashirika, na makuhani wa kilimwengu wanaoniheshimu kwa njia hii maalumu, ulinzi wangu maalumu, ongezeko la miito ya kiroho, na utakatifu mkubwa miongoni mwa watumishi wa Mungu."- Maneno ya Bikira Maria Rosa Mystica, Juni 13, 1947

Katika mfululizo wa matokeo haya, Bikira Maria alijidhihirisha kwa Pierina akiwa amevaa mavazi yote meupe; katika gauni refu na joho lenye kofia. Kilicho kuwa cha ajabu kuhusu maonyesho haya ni maua matatu ya waridi yalionekana yamechanua moja kwa moja kutoka kifuani mwa Bikira Maria, waridi la kwanza ilikua waridi nyeupe, waridi la pili ilikuwa waridi nyekundu na tatu ilikuwa waridi ya njano, ambayo kulingana na mtokewa Pierina, yalionyesha "moyo" wa ufunuo wa Mama Yetu : waridi hizo ziliwakilisha SALA (Waridi Nyeupe); SADAKA (Waridi Nyekundu); TOBA (Waridi Njano).

mama maria

Mnamo Aprili 17, 1966, baada ya kuishi kwa kujitenga kwa karibu miaka 20, Pierina alikwenda kwenye kijito kilicho pembezoni mwa Montichiari, mahali panapoitwa Fontanelle, ambapo Bikira Maria alikuwa amemwongoza aende. Huko, Mama Mwenye Heri alijitokeza na kubariki maji kwa nguvu za uponyaji. Pia aliomba kanisa dogo lijengwe kwenye eneo hilo, pamoja na hilo aliomba huduma za sala na maandamano yafanyike maeneo hayo kila Julai 13  hasa kwa jina lake kama Maria, Rosa Mystica. Ishara na maajabu yalitokea wakati wa matokeo katika eneo hilo – uponyai wa watu wengi, harufu nzuri ya mbinguni, na siku nyingine jua lilionekana likicheza – na miujiza mingi mpaka leo inaendelea kuripotiwa.

Pierina Gilli alikufa Januari 12, 1991, baada ya kuishi maisha ya mfano ya ibada ya unyenyekevu na utii kwa viongozi wa kanisa la eneo hilo. Baada ya kutimiza utume wake wa umma, alikaa mbali na kanisa  la Fontanelle, kwa maelekezo ya askofu wake, lakini bado alikaribisha mahujaji waliokuja kwenye kanisa dogo katika nyumba yake. Pierina pia alikuwa dhahiri ni Roho-Mteseka na inasemekana aliteseka kwa madonda ya Yesu  yasiyoonekana..

Mnamo Desemba 7, 2019 Askofu wa Brescia - Monsinyo Pierantonio Tremolada - chini ya mamlaka yake Fontanelle iko, aliteua Kikanisa  cha Rosa Mystica kuwa Sehemu ya Kanisa la Jimbo hilo rasmi chini ya jina zuri la Rosa Mystica-Mama wa Kanisa.

Kuanzia Julai 5, 2024, kwa kujibu Barua iliyowasilishwa na Askofu Pierantonio kwenda Vatican, Dicastery ya Mafundisho ya Imani ilitoa idhini rasmi ya tathmini yake chanya ya matunda ya kiroho ya matokeo na ujumbe wa Rosa Mystica huko Montichiari-Fontanelle. Kwa hivyo, maonyesho haya sasa yanachukuliwa kuwa moja ya matokeo machache yaliyoidhinishwa rasmi na kutambuliwa na Roma! Shukrani na Sifa kwa Mungu!

 

Post a Comment

0 Comments